DAMIJA MK MAKENE MICHUZI MWANDANI NDESANJO CHARAHANI AISHA ABDI MAVAZI SHAMIM MAGGID WATANZANIA Jumuia ya Wanablogu wa Tanzania
UNO AU EAC TANZANIA EU NASA REUTERS IPP Muungano wa Vijana Duniani dhini ya UKIMWI TIG IPP
NITUMIE BARUA PEPE

Kimya Kingi ..............
Saturday, May 06, 2006


Amani na Uhuru wa kweli viwe nanyi nyote ndugu zangu. Naandika waraka huu nikiwakumbuka ndugu zangu ambao nimewatupa kwa muda mrefu sana hapa kwenye blogu.

Maisha ni safari, kwa maana hiyo wote tunaoishi hayo maisha basi ni wasafiri. Msemo huu ninausema ukiwa na muktadha wa kuwajulisha wenzangu juu ya mikasa iliyonikuta katika hizo harakati zangu za safari ya maisha. Najua kutokana na kutokuwa na taarifa wengi wenu mmekuwa mkijiuliza huyu Bw. mdogo vp? Mbona haeleweki!!

Kwanza, kabisa nilitingwa sana sana na masuala ya kifamilia kiasi kwamba nilikuwa nakosa kabisa muda wa kuingia mtandaoni.

Lakini pia, mnamo tarehe 2-04-2006 siku ya Jumamosi majira ya saa kumi na mbili asubuhi, nilipatwa na mkasa ambao hata sijui nisemeje. Nimetoka nyumbani maeneo ya Kinondoni B salama salimini, nikapanda daladala ya kuelekea buguruni, nikashuka kituo cha Magomeni Mikumi, nikavuka barabara, huyoo kiguu na njia naelekea ofisini kwangu pale Kituo cha Msaada wa Sheria Magomeni. Wakati nakatiza barabara ya kuingilia soko la Magomeni nyuma yangu kulikuwa na kundi la vijana karibu sita wakija pia katika uelekeo wangu, ghafla nikajikuta nimepigwa roba ya nguvu maana majamaa yalikuwa mashababi kweli kweli huku wakianza kazi ya kunisachi kama nina chochote kile kwa ajili yao, nami nikaanza harakati za kujihami, basi kilichoendelea hapo nimekuja kuhadithiwa siku ya pili. Baada ya kisanga kile ambacho kilichukuwa takriban dakika kumi hivi, nilitolewa pale eneo la tukio na raia wema na kupelekwa hadi ofisini ambapo taratibu zilifanyika na wafanyakazi wenzangu kunipeleka pale kituo cha Polisi Usalama Magomeni, ambapo nilipatiwa PF 3 na kupelekwa mwananyamala hospitali ambapo nilipewa rufaa mpaka Muhimbili, siku hiyo fahamu zilinirejelea baada ya angalau masaa sita hivi tangu alfajiri ile. Wale jamaa hawakufanikiwa kunichukulia chochote kile kati ya vitu ambavyo nilikuwa navyo mfukoni yaani simu na hela kidogo ila wameniachia jeraha litakalonikaa moyoni kwa muda mrefu kiasi. Wameniumiza sana sana jicho langu la kulia kasi kwamba kwa sasa halioni vizuri kabisa. Nimefanya X-Ray karibu sehemu zote muhimu mwilini na kukutwa niko salama jambo ambalo kwalo namshukuru sana mola.

Nimetoka hospitali siku ya J'mosi ya tarehe 29 -04-06 jioni na nimeanza kuja kazini rasmi leo J'mosi ya tarehe 06-05-06.

Lakini pia nikiwa hospitali nilitumia muda huo kutathmini ushiriki wangu kwenye kuendelea hili gurudumu la blogu na kujipanga upya katika uwasilishi wa yale yaliyo moyoni mwangu katika kujenga jamii chanya. Kwa kuanzia, nitakuwa nikiandika kwa mrengo ule ule nilioanza nao awali, pia nitakuwa nikiandika kwa juma mara moja ambapo kwa kuanzia nimeonelea siku ya J'tano kuwa ni siku muafaka kwangu kutoa muktadha ambao nitakuwa nimeukusanya kwa takriban juma lote.

Safari ya maisha bado inaendelea! Tuonane juma lijalo!!!!!
Muandishi: Kaka Poli Saa: 10:54 am | Permalink |


5 Comments:


 • Saa: Saturday, May 06, 2006 6:26:00 pm, Mtoa Maoni: Blogger Boniphace Makene

  Pole ndugu yangu Pori, pole sana, hawa jamaa hawafai ndugu yangu, umaskini si kigezo cha kuchukua kila kitu cha watu kwa nguvu! Sioni sababu ya jamii yetu kuamua kuchukua tabia hii ya kutumia nguvu bila kutambua kuwa wanaooumizwa ni binadamu kama wao. Awali nilipoona picha hizi nikadhani na wewe ulikuwa katika mkasa ule wa Ubungo lakini kumbe akili yangu ilikuwa karibu kabisa na ukweli huu. Pole sana Mola atakujalia utapona kabisa na kuendelea kuandika humu nasi.  
 • Saa: Monday, May 08, 2006 6:54:00 am, Mtoa Maoni: Blogger ned

  Mzee,
  Pole sana kwa mkasa... Maisha ndio hivyo - wanasema "hujafa, hujaumbika" Mkasa kama huoni msiba - ambao kama unavyojua huwa haubishi hodi. Naungana na Makene kukuombea Mungu uponyaji wa haraka na amani moyoni - unajua tena... "aliyeumwa na nyoka....."

  Ned  
 • Saa: Monday, May 08, 2006 4:16:00 pm, Mtoa Maoni: Blogger mwandani

  Pole sana  
 • Saa: Wednesday, May 10, 2006 2:53:00 pm, Mtoa Maoni: Blogger Egidio Ndabagoye

  Pole sana kaka  
 • Saa: Thursday, February 08, 2007 7:15:00 pm, Mtoa Maoni: Anonymous Anonymous

  Pole sana ndugu yangu. Nakutakia upone haraka na ujiimarishe tena kimwili na kiakili.

  Masalaam,

  F MtiMkubwa Tungaraza.  
eXTReMe Tracker