DAMIJA MK MAKENE MICHUZI MWANDANI NDESANJO CHARAHANI AISHA ABDI MAVAZI SHAMIM MAGGID WATANZANIA Jumuia ya Wanablogu wa Tanzania
UNO AU EAC TANZANIA EU NASA REUTERS IPP Muungano wa Vijana Duniani dhini ya UKIMWI TIG IPP
NITUMIE BARUA PEPE

Thursday, February 09, 2006
Habari za leo wote!

Naomba niweke IGIZO aliloliweka Kaka yangu mti Mkubwa kupitia kwa mwanablogu mwenzetu Damija.


Hivi majuzi Dennis Londo na MtiMkubwa kupitia kwa damija walituletea kisa cha Mchina kumtwanga Mtanzania hadi kumuua. Leo katika kidirisha cha maoni nimekutana na onyesho kamili la jinsi hali ilivyokuwa, nimeona niwaletee wote tushirikiane kuona hali halisi ya Watanzania tulivyo. Kwa mtindo huu tusije shangaa kukuta 'Mti' kaamua kututengenezea kabisaa filamu yake. Haya onyesho lenyewe hili:-


SEHEMU YA KWANZA:
Mchina mfupi, mdogo kwa umbo, na sura yake kama paka anaonekana anamkimbiza Mtanzania. Mtanzania anakimbia kwa mbio zake zote huku anageukageuka nyuma kuangalia kama atadakwa. Mchina anaongeza kasi. Mtanzania maskini wa MUNGU kasi inapungua kadri anavyozidi kukimbia. Hatimaye Mchina anamkamata Mtanzania.Wakati huo huo wa kumkimbiza Watanzania wengine wanakimbilia nyuma. Siyo kwamba wanakimbilia kumdhibiti Mchina isipokuwa wanakimbilia kuona kibano atakachopewa Mtanzania na Mchina.


SEHEMU YA PILI:
Mchina kamkamata mwizi wake (Mtanzania). Wote wawili wanahema kwa nguvu kwa sababu ya kukimbia. Mchina anamkunja shati Mtanzania. Watanzania wengine wamefika kwenye tukio wanasubiri kuona cha mtema kuni atakachokipata Mtanzania mwenzao. Mchina anaanza shughuli ya kumuadabisha Mtanzania kwa vibao. Kwa kila kibao anachopokea Mtanzania analia "..mama!.." "..ang'i!.." "..mama!.."Wakati huo Watanzania wengine wanashabikia "..Kula eeeh.." "..kula eeeh.." "..k...mae wallai Wachina siyo mchezo cheki anavyopiga kunfuu.." Mchina anaona anaumiza mkono wake kwa sababu jamaa ni sugu sana anachukua chuma anaanza kumbonda nalo kichwani kama anaua nyoka. Mtanzania damu zinamchuruzika kwa majeraha. Watanzania wengine wanaacha kuangalia wengine wanaangalia huku wakisema "..Mchina akikasirika hatari.." "..hawa jamaa huwa hawaongei lakini 'usiwauzi'..Maanake wakikasirika jasho litakutoka.." Mchina anaendelea kubonda kichwa na nondo. Paa la uso linapasuka. Mtanzania sasa halii tena bali anaguna tu kila pigo la nondo likitua "..mmgh.." Pigo jingine "..mmmgh.." na jingine tena "..mmgh.." na jingine tena "..mmgh.." na jingine tena hakuna sauti inayotoka Mtanzania kishapoteza fahamu. Mikono, viatu na nguo za Mchina vimetapakaa damu ya Mtanzania. Mchina anamuangalia mtuhumiwa wake anaridhika na kisago alichompa.


ONYESHO LA TATU
Mchina na wenziye wanachumpa ndani ya gari yao kwenda kunawa na kubadilisha nguo. Watanzania waliokuwepo kwenye tukio wanaondoka wasije wakakutwa na polisi wakatakiwa kutoa ushahidi. "..haroo, yaani yule Mchina arikuwa kakasirika bwana..Maanake arikuwa anampiga kwa nguvu kama nini.." "..Mshikaji tukijikate mandata wasije wakatukuta hapa tukaitwa kwenye ushahidi.." "..Lakini jamaa kajitakia mwenyewe sasa kwa nini aliiba?.." ".unajua mimi nilianza kuwaona tangu wanamkimbiza, nikajua tu leo jamaa ataipata.." "..Hivi arifikiri anaweza kumshinda mbio Mchina..Wachina wanafanya mazoezi ware tangu wadogo.." "..Mimi nirikuwaga nawaonaga wakati wanajenga reri ya tazala, tujamaa tudogo rakini tunabeba mataruma ya reli kama kanabeba rura ya kupigia mistari.."


ONYESHO LA NNE
Mtanzania mmoja mzalendo aliyekereheshwa na kitendo kizima anakwenda kuita polisi baada ya tukio kuisha. Polisi wanakuja na mwandishi wa habari mmoja. Polisi wanampinduapindua maiti. Halafu wanawaamrisha watu "..Hebu sogeeni mbali mnatunyima nafasi.." Polisi mmoja anachapa chapa virungu watu wanasogea mbali kidogo. Wengi wa watazamaji wa tukio ni wanaume vijana na watoto wadogo. Watoto wengine wanamtazama maiti huku macho yamewatoka kama wanatazama sinema ya dracula. Polisi wanampindua marehemu kutoa kitambulisho mfukoni ili kumjua jina lake. Kwa bahati nzuri ana kitambulisho. Wamemtambua jina. Halafu wanampasia mwandishi wa habari kitambulisho. Mwandishi anachukua jina halafu anamrudishia ofisa. Maiti anaokotwa anawekwa nyuma ya Land Rover anapelekwa hospitali. Watanzania wanatawanyika. Eneo la tukio linaachwa na damu halafu polisi wamesahau kuokota nondo iliyotumika kumpigia marehemu. Msamaria mwema anaiokota anaitupa jalalani huku akisema "..Isije ikaua mwingine.."


MWISHO
Mchina anapigiwa simu aende kituoni akatoe maelezo ya tukio. Kituo yupo ofisa upelelezi kesi za jinai. Kiingereza chake siyo kizuri sana kwa hiyo stetimenti ataiandika Kopla Masanja kwa sababu anaongea Kiingereza kizuri zaidi. Mchina anafika kituoni masaa kadhaa baada ya tukio. Stetimenti inaandikwa. Mchina anaambiwa itabidi alale ndani jioni ya leo. Baada ya siku mbili tatu suala linakuwa kati ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Ubalozi wa China nchini Tanzania. Kwa sababu za kidiplomasia Mchina anakuwa 'dipotedi' Kesi imekwisha.

Watanzania hivi sivyo inavyokuwa? Kama nimekosea kutengeneza onyesho niambieni! Sawa?
Muandishi: Kaka Poli Saa: 2:36 pm | Permalink |


3 Comments:


eXTReMe Tracker