DAMIJA MK MAKENE MICHUZI MWANDANI NDESANJO CHARAHANI AISHA ABDI MAVAZI SHAMIM MAGGID WATANZANIA Jumuia ya Wanablogu wa Tanzania
UNO AU EAC TANZANIA EU NASA REUTERS IPP Muungano wa Vijana Duniani dhini ya UKIMWI TIG IPP
NITUMIE BARUA PEPE

IGIZO HALIJAISHA ....!!
Monday, January 30, 2006
'Heshima na ufahari viwe juu yenu nyote wanablogu wapya na hata wale wa zamani pia. Kwa masikitiko makubwa kabisa, nawaomba radhi kwa kuchemsha kupata maneno ya kiswahili ya 'episode' na 'scene' ili niweze kuweka hoja katika muktadha.

Majimbo, Wabunge, Walalahoi na Maslahi ndio muktadha ninaouweka kwenu hadhira ya blogu hii leo, yaani hi ni kwa wote wale wasomaji tu, wasomaji na wachangiaji na hata wachagizaji pia. Fanani wenu leo nimekumbuka kwamba kumbe lile igizo ambalo Idya Nkya na wengine kadhaa ambao tulidhani limekwisha, basi tulipotea kudhani vile kwani ile ilikuwa ni 'episode' ya kwanza ya igizo lenyewe.

Majuma kama mawili hivi yaliyopita igizo liliendelea na hii ndio 'episode' yenyewe. Wabunge wa Bunge la 'Jamhuri' ya Muungano wa Tanzania, wakiwa katika semina ya Wabunge pale katika ukumbi wa Karimjee Dar es Salaam walileta hoja nzito na tete ya kutaka kuongezewa maslahi 'marupurupu' zaidi ya viwango vilivyopo sasa kwa Wabunge. Hoja hiyo pia ilisindikizwa na kuongezwa kwa kipindi cha Ubunge kutoka miaka mitano kama ilivyo sasa hadi miaka saba. Hiyo hoja ya kuongezewa muda japo haijawa tete sana lakini mimi naipa uzito wake wa hali ya juu. Kwa mfano, ndani ya hilo Bunge la sasa hivi kuna wabunge kadhaa ambao vipindi walivyokaa bungeni na zaidi ya miaka 15 na wengine ni zaidi ya miaka ishirini, sasa kuna swali najiuliza, Mbunge yupo Bungeni akiwakilisha jimbo moja tangu miaka ya 70 mpaka leo hii, na hakuna mabadiliko chanya aliyoyafanya jimboni kwake, bado anahitaji kuongezewa muda? Dhamira ya mabadiliko ya kimaendeleo si suala la mtu tu kujiamulia bali ni utashi wa mhusika wa dhamira hiyo. Naomba nimpe 'tano' Mh. Nimrod Mkono mbunge wa jimbo la Musoma Vijijini kwa kujitolea kwake katika kuleta maendeleo jimboni kwake. Zaidi ya kuwa mbunge kwa kipindi cha 2000/2005 sidhani kama aliwahi kuwa mbunge tena. Lakini yanyosemwa kuhusiana na maemdeleo ya jimbo lake ni chanya tupu, huyu bwana hata wapinzani walimpigia ndogondogo ya kupewa nafasi ya kuendeleza na yale ambayo ameyadhamiria katika kuleta maendeleo kwa watu wa Musoma Vijijini.

Suala la kuongezewa maslahi limeamsha hisia za wengi miongoni mwa wanajamii katika nchi hii ya wadanganyika. Wabunge wanataka ongezeko la posho za vikao vya Bunge kutoka Shilingi laki moja wanayopata sasa, ongezeko la mshahara kutoka Shilingi milioni moja na laki mbili wanazolipwa sasa, na posho ya jimbo ambayo ni shilingi milioni moja, akimaliza kipindi chake cha miaka 5 ya ubunge analipwa kiinua mgongo cha Shilingi milioni thelathini.


'Episode' hii ndio haswa ninayoijadili leo. Kwanza kabisa naomba niwakumbushe wenzangu hapa nyumbani na ughaibuni pia; kima cha chini mshahara kwa Mtanzania 'mwanajimbo' si zaidi ya Shilingi sabini elfu kwa mwezi, madaktari wanadai nyongeza ndogo tu ya mshahara, wabunge wetu kwa asilimia kubwa kabisa hawakai kwenye majimbo yao wanayoyawakilisha bungeni na ni nadra sana pia kuonekana kwenye hayo majimbo mara wanapopata ubunge. Hawajui ukweli wa matatizo yanayowakabili hao waliowapa hiyo 'kula'. Wabunge wetu kwa kweli wameanza kuonyesha uhalisia wao wazi wazi, wamesahau kutueleza mikakati na vipaumbele katika kutatua matatizo yanayowakabili wananchi huko majimboni na kukurupuka kudai fidia ya mitaji waliyoiwekeza katika kutafuta huo ubunge wenyewe. Hii ni ishara tosha yenye kuonyesha dira ya miaka mitano ya hawa wabunge wetu. Wanadai posho katika kipindi ambacho nchi imekumbwa na baa kubwa la njaa, na sikumsikia wala kusoma popote pale ambapo Mbunge huyu ameomba ruhusa kwenye hiyo semina ili kwenda kuwatembelea wananchi wanaokaribia kufa na njaa huko majimboni mwao! Wakati ambapo wanadai nyongeza hiyo, wengine watakwenda tu kusinzia to bungeni, sijui na sisi tuwadai kodi ya matumizi mabaya ya rasilimali za bunge kwa kugeuza viti kuwa vitanda?
Muandishi: Kaka Poli Saa: 5:28 pm | Permalink |


1 Comments:


eXTReMe Tracker