Ni takriban miezi tisa sasa tangu nilipoanza kuperuzi blogu mbali mbali duniani. Kwanza iliniwia vigumu sana kuelewa maana halisi ya blogu, lakini kadiri siku zilivyozidi kusonga mbele bila kutusubiri akina sisi nilianza kwa taratibu kuelewa nini haswa lengo la blogu. Nimesoma blogu nyingi na kwa mra kadhaa kujaribu kutengeneza lakini kutokana na teknolojia hii kuwa ni mpya kabisa, iliniwia vigumu kwa kipindi chote hicho kuweza kutengeneza hiyo blogu yangu. Na hata zile ambazo nimejaribu kuzitengeza sikumbuki tena viunga vyake. Nilihamasika zaidi baada ya kuanzishwa kwa hizi blogu za Kiswahili, nakumbuka blogu ya kwanza kukutana nayo kwa lugha hii ni ya Kaka yangu
Ndesanjo ambayo nilipitia moja makala zake zinazotoa maelekezo ya namna ya kunzisha blogu na kwa kiasi fulani nikafanaikiwa kuanzisha hii
blogu yangu.
Madhumuni ya blogu hii ni kama kichwa chake kinavyosomeka "Mtandao wa Mawazo na Habari Chanya". Katika upashanaji habari kuna njia mbalimbali ambazo mpashaji na yule anayepashwa huzitumia. Habari yoyote ile inapotolewa, ni lazima itakuwa na lengo la kutolewa kwake. Kwa kipindi kirefu sana, Watanzania tumekuwa tukimezeshwa habari hasi zenye lengo la kutuondoa katika upekuzi na utafiti huku tukibaki na mapukupuku ya ujinga yatokanayo na utandawazi.
Tumetawaliwa kiakili kiasi kwamba tumesahau kabisa sisi ni akina nani. Sasa basi, kwa kupitia blogu hii, tutaamshana, kukumbushana na kupeana hamasa ya kujitambua kwa kupeana habari chanya na mawazo jengevu. Ili tuweze kujenga jamii chanya, tunahitaji umoja, mshikamano, kujielewa na kuelewana, kuhabarishana, n.k. Nipo nanyi nyote na ninaomba kujiunga nanyi.
NIMEPIGA HODI, BILA SHAKA NITAKARIBISHWA!!!!!!!! HONGERA WANABLOGU WOTE WA KISWAHILI!!
Karibu tupo.